New
Upelelezi wa Yule Binti aliyejitosa baharini umefikia hapa...
Wakati Polisi Zanzibar ikisema imekamilisha kumhoji msichana aliyejitosa Bahari ya Hindi eneo la Chumbe alipokuwa akisafiri na boti ya Kilimanjaro (V) kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, mtaalamu anasema binti huyo amethirika kisaikolojia ni bora angeachwa apumzike.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali aliliambia gazeti hili jana kuwa, msichana huyo anayesoma kidato cha tatu Sekondari ya Glorious na watu wengine wameshahojiwa kuhusu tukio hilo la Aprili 3.
Hassan alisema miongoni mwa walihojiwa ni wanafamilia, msichana huyo na manahodha wa boti ya Kilimanjaro ambao walimuokoa.
Alisema polisi imepata taarifa kamili juu ya tukio hilo, hivyo wakati wowote jalada litafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda Hassan alisema kazi kubwa ya polisi ilikuwa ni kufanya utafiti wa awali juu ya tukio hilo, kujua historia ya msichana huyo.
Msichana huyo alihojiwa na polisi baada ya daktari aliyefanya uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Kidongo Chekundu, kuruhusu baada ya kuridhika na hali yake kuimarika.
Hata hivyo, Mratibu wa Huduma za Afya Mjini Unguja, Suleiman Abdi Ali aliyemhudumia msichana huyo alibainisha kuwa aliathirika kisaikolojia baada ya tukio hilo, hivyo isingekuwa vyema kwa polisi au ndugu na jamaa kumhoji.
Mama mdogo wa msichana huyo, Asha Saleh Manzi akizungumza na gazeti hili jana, alisema hali ya afya ya mtoto wao si nzuri tangu tukio la kujirusha baharini.
Asha alisema kutokana na hali hiyo ya afya, wamemsimamisha kwenda shule ili apate tiba zaidi.
Alisema wametumia dawa za hospitali kama yalivyo maagizo ya daktari, lakini amekuwa akiweweseka na kuna wakati hutoka ndani na kukimbilia baharini.
No comments:
Post a Comment