About me

Technology

Monday, January 9, 2017

Wataalamu Wataja Sababu za Ongezeko la Wanawake Wanaokunywa Supu ya Pweza


WAMECHARUKA! Baada ya wanaume kusifika kuwa ndio wateja wakubwa wa minofu ya samaki aina ya pweza na supu yake, hali sasa imebadilika baada ya kinadada kuonekana pia wakichangamkia kwa wingi bidhaa hiyo.

Uchunguzi wa Nipashe katika maeneo maarufu ya uuzwaji wa pweza na supu yake jijini Dar es Salaam, unaonyesha kuwa kwa sasa, tofauti na vile ilivyozoeleka, kinadada na kinamama wamekuwa wakijumuika na wanaume katika kumla pweza na pia kunywa supu yake.

Maeneo yaliyohusishwa zaidi katika uchunguzi huo ni pamoja na stendi ya Makumbusho, Mwenge, Tegeta, Ubungo, Mbezi Luis, Buguruni, Tandika na Mbagala.

Nipashe imebaini kuwapo kwa wateja wanawake wanaofika kwa idadi kubwa katika maeneo wanayouza pweza na kujumuika na wateja wengine katika kuchangamkia bidhaa hiyo, tofauti na ilivyokuwa awali.

Kwa wastani, kupitia wauzaji waliozungumza na Nipashe, imebainika kuwa kuna ongezeko la takribani asilimia 40 ya wateja wanawake, hiyo ikitokana na wastani wa kuwa na wanunuaji walau wanne katika kila wateja 10.

Awali, ilielezwa na wauzaji wengi kuwa haikuwa ajabu kutopata mteja wa kike walau mmoja wa supu ya pweza kwa siku.

Katika uchunguzi huo, Nipashe imebaini kuwa wako kinamama walioonekana kujiandaa zaidi kwa kufika na vifaa vya kubebea supu, zikiwamo chupa za maji zilizotumika huku baadhi yao wakifika kwa wauzaji  na vifaa vya kubebea supu, zikiwamo chupa za maji zilizotumika huku baadhi yao wakifika kwa wauzaji wakiwa na bakuli maalumu za vyakula maarufu kama ‘hotpot’, chupa ya chai na kuwekewa supu na finyango za samaki huyo.

Wanaume ndiyo waliokuwa wakisifika kwa ulaji wa supu ya pweza uliopamba moto zaidi jijini Dar es Saalam katika miaka ya hivi karibuni kutokana na taarifa kwamba pweza husaidia mambo mengi mwilini, hasa katika kuimarisha urijali.

Baadhi ya wauzaji wameiambia Nipashe kuwa hali sasa iko tofauti sana kwa sababu wanawake ni miongoni mwa wateja wao wazuri kwa sasa.

“Tena wapo kinadada hawakosi kunywa supu ya pweza walau mara tatu kwa wiki. Wapo pia ambao kila wanapokuja hunywa hadi vibakuli vitatu vya supu na pia kutafuna minofu yake,” mmoja wa wauzaji katika eneo la Makumbusho aliiambia Nipashe.

Muuzaji mwingine katika eneo la Ubungo alisema kabla, alizoea kupata wateja wachache wanawake na kwamba, wengi wao walikuwa wakiomba kufungiwa tu vipande vikubwa vya mikia ya pweza na kuondoka navyo; hali ambayo hivi sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa sababu idadi yao wale wanaofika kununua hivi sasa imeongezeka.

“Kama unavyoona mwenyewe… biashara hii tunaifanya sana kuanzia mida ya saa moja usiku na kila ukija utawaona kinadada na kinamama wakiwa sehemu ya wateja wetu. Tunashukuru sana kwa elimu inayoendelea kutolewa kuhusu faida za pweza mwilini na hilo limechangia kutuongezea wateja na kukuza mitaji yetu,” alisema muuzaji mwingine katika eneo la Mbagala, aliyejitambulisha kwa jina moja la Salum.

Muuzaji mwingine katika eneo la Mwenge, alisema kwa eneo analouza yeye, anakadiria kuwa wateja wanaume na wanawake hufika kwa uwiano sawa.

“Hapa kwangu, wateja wanawake na wanaume hawapishani kwa idadi… kwa wastani, katika kila wateja 10, watano huwa ni wanawake,” alisema muuzaji huyo, akiongeza kuwa umaarufu wa pweza na faida zake kwa walaji unaweza kuwa chanzo cha kuongezeka kwa walaji kinadada katika siku za hivi karibuni.

SABABU KUONGEZEKA WATEJA WANAWAKE

Wakizungumza na Nipashe, wauzaji wengi walidai kuwa kuenea kwa taarifa za wataalamu zinazothibitisha ubora wa virutubisho vya samaki pweza ndiyo sababu ya kuvutika kwa wanawake wengi zaidi katika utumiaji wa samaki huyo.

“Pweza huliwa kwa idadi sawa majumbani. Lakini haikuwa kawaida kuwaona kinadada katika maeneo haya ya wazi tunayouza vipande vya samaki huyo vilivyokaangwa au kuchemshwa pamoja na supu yake.

Haya ni mabadiliko makubwa yenye faida kwetu kwa sababu wateja wanazidi kuongezeka,” alisema muuzaji mmojawapo katika eneo la Tegeta, aliyedai kwamba kwa siku huingiza faida ya hadi Sh. 25,000 kutokana na biashara yake hiyo.

Mmoja wa kina dada waliokutwa wakipata huduma ya supu ya pweza eneo la Makumbusho na kujitambulisha kwa jina moja la Joyce, aliiambia Nipashe kuwa yeye alianza kuwa mlaji mzuri wa pweza miaka minne iliyopita baada ya kujifungua na kubaini maziwa hayakuwa yakitoka vizuri, lakini alipotekeleza ushauri wa kula pweza usiku na mchana, haikumchukua muda mrefu kupata nafuu ya tatizo hilo.

“Na tangu hapo nikawa miongoni mwa walaji wakubwa wa pweza kwa sababu nilikuja kuelezwa faida zake nyingine nyingi kiafya. Hata hivyo, kwa sababu ya kazi, sipati nafasi ya kujiandalia mwenyewe na ndiyo maana huwa nakula walau kidogo kwenye maeneo wanayouza mitaani,” alisema Joyce.

DAKTARI ANENA

Akizungumza na Nipashe kuhusu faida za pweza na taarifa za kuwapo kwa ongezeko la wateja kinamama, Dk. Damas Mahenda, Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alisema ni kweli samaki jamii ya pweza wana faida nyingi mwilini, hivyo si ajabu kusikia watu wakichangamkia matumizi yake, wakiwamo kinamama.

Dk. Mahenda alisema samaki jamii ya pweza wamejawa na virutubisho vinavyosaidia mengi ikiwamo kuongeza ashki na kuboresha tendo la ndoa huku pia minofu ya samaki huyo ikiwa na virutubisho vya kumuwezesha mwanamke kuwa na sifa halisi za ‘ukike’ na pia mwanaume kuimarika afya yake.

Alivitaja baadhi ya virutubisho vingi vinavyopatikana kwenye mlo wa supu au minofu ya pweza kuwa ni pamoja na protini, mafuta (fats), vitamini B12, selenium, madini chuma (iron), shaba na pia vitamini B6.

“Virutubisho vyote hivi vinapatikana kwa kiasi kikubwa kwenye minofu ya pweza na karibu vyote ni muhimu katika mwili wa binadamu,” alisema Dk. Mahenda.

“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa pweza ana faida nyingi. Na kwa ufupi, unaweza kumuelezea pweza kwa kumlinganisha na kifurushi cha virutubisho muhimu vya mwili wa binadamu. Mnofu wa pweza una protini nyingi kuliko wa kuku. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 10 ya virutubisho protini nyingi kuliko wa kuku. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 10 ya virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini kwa siku hupatikana kwa pweza aliyeivishwa vizuri,” Dk. Mwindah Abdallah wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) aliwahi pia kuiambia Nipashe kuhusu faida za pweza, jambo linalochangia kuongezeka kwa walaji wake wakiwamo wanawake kadri taarifa zinavyozidi kuwafikia wengi.

Aidha, kupitia mahojiano na Dk. Mahenda, Nipashe ilibaini kuwa faida nyingine za pweza zinazovutia walaji wengi kila uchao ni pamoja na kuwa na virutubisho vya selenium vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nguvu ya tendo la ndoa wanaume na wanawake na pia vipo vinavyosaidia kuwaongezea wanaume idadi ya mbegu (sperm count).

“Kwa sababu hiyo, supu ya pweza iliyoandaliwa vizuri inaweza kuwasaidia wanandoa katika kukamilisha jukumu lao la unyumba kwa namna bora zaidi,” alisema Dk. Mahenda.

Faida nyingine ni ya virutubisho vya pweza ni kusaidia mwili kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali ya saratani zikiwamo za midomo, tumbo, utumbo mkubwa, matiti, shingo ya kizazi, na pia saratani ya mapafu; kuukinga mwili dhidi ya kupungukiwa kwa uwezo wa ubongo hasa kwa watu wenye umri mkubwa (Alzheimer); husaidia walaji kukabili athari za maradhi ya pumu; kuongeza uzalishaji wa haemoglobin ambazo ni muhimu katika damu na hiyo ni kwa sababu pweza ana madini mengi aina ya shaba na pia kupunguza athari za baadhi ya maradhi ya moyo kwa sababu ya kuwapo kwa kiwango cha mafuta aina ya ‘omega­3 fatty acids’.

Hata hivyo, licha ya faida nyingi za supu ya pweza na minofu yake mwilini, Dk. Mahenda alitahadharisha juu ya athari hasi zinazoweza kujitokeza kwa baadhi ya walaji wa pweza kuwa ni pamoja na kushambuliwa na mzio (aleji).

Nipashe imebaini vilevile kuwa ripoti za tafiti nyingine kuhusiana na ulaji wa pweza zinaonya kuwa samaki huyo hapaswi kutumiwa sana na kina mama wajawazito kwa sababu anaweza kusababisha athari zitokanazo na madini ya zebaki ambayo hupatikana pia mwilini mwake, ijapokuwa huwa ni kwa kiasi kidogo.

Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Popular Posts